Thursday 1 August 2013

NCCR yaigaragaza tena CCM kortini


Chama cha NCCR-Mageuzi kimeendelea kuigaragaza CCM mahakamani, baada ya Mbunge wa Kasulu Vijijini, Mhe. Agripina Zaituni Buyogela (pichani), kuibuka kidedea kwenye rufaa ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, yaliyompa ushindi.
Hiyo ni mara ya pili kwa Buyogela, kuibuka kidedea dhidi ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Daniel Nsanzugwanko, aliyekuwa akigombea kiti hicho kupitia CCM.
Nsanzugwanko, alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora akipinga matokeo yaliyompa ushindi Buyogela.
Licha ya mambo mengine, Nsanzugwanko alilalamikia mwenendo mbaya na ukiukaji wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, huku akimtuhumu Buyogela kuendesha kampeni chafu, kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi yake, kuwa ni mchawi aliyeua watu na mwizi. Alidai kwenye mikutano yake, Buyogela alimtuhumu kuwa aliwaua Wabunge wa zamani wa jimbo hilo, Bernard Machupa na Teddy Magayane.
Hivyo, aliomba mahakama hiyo itengue matokeo yaliyompa ushindi na kuamuru ufanyike uchaguzi mdogo, au imtangaze yeye kuwa mshindi. Hata hivyo, Mei 3, 2012, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Haruna Songoro, alitupilia mbali madai ya Nsanzugwanko akisema ameshindwa kuyathibitisha pasipo mashaka yoyote.
Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Nathalia Kimaro, Salum Massati na William Mandia, walikubaliana na hoja za mawakili wa utetezi na kuamua kutupilia mbali rufaa hiyo.
Habari hii imeandikwa na James Magai wa gazeti la Mwananchi.

No comments:

Post a Comment